
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ofisi ya Kanda ya Kaskazini , kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali ikiwemo Watoa Huduma wa Mitandao ya Simu (MNOs) na Vyombo vya Habari imeanza kampeni ya kutoa elimu kwa umma kuhusu kusitisha matumizi ya kadi za kukwangua za muda wa maongezi na kuhamia kwenye njia za kidijitali za kuongeza muda wa maongezi.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na TCRA tarehe 8 Oktoba 2026, shughuli za uhamasishaji zilianza tarehe 1 Oktoba 2026, huku zoezi la majaribio la kusitisha matumizi ya kadi hizo likipangwa kuanza tarehe 1 Januari 2027 katika maeneo maalumu ya mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Mwanza na Mbeya.
Tarehe ya utekelezaji wa mpango huo kitaifa itatangazwa baadaye.

Akizungumza na Malunde 1 Blog, Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Kanda ya Kaskazini Mhandisi Francis Mihayo amesema kuwa Zoezi la majaribio la kusitisha matumizi ya kadi za kukwangua za muda wa maongezi ya simu litaanza tarehe 1 Januari 2027 katika Mkoa wa Arusha: Jiji la Arusha, Wilaya ya Arusha, Meru na Karatu.
Akijibu Maswali ya Mwandishi wa Malunde 1 blog alitoa ufafanuzi ufuatao:-
Kwa nini TCRA inapendekeza kuhamia kwenye mfumo wa kuongeza muda wa maongezi kidijitali ?
Serikali imeendelea na jitihada mbalimbali za kupunguza matumizi ya fedha taslimu katika uchumi (cashless economy) kwa lengo la kuongeza matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali, kuongeza uwazi wa miamala na kurahisisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Katika kutekeleza suala hilo, Wizara ya Fedha kupitia Bajeti ya Kuu ya Serikali ya Mwaka 2026/27 pamoja na Amri ya mwaka 2026 chini ya Sheria ya Miamala ya Kielektroniki, Sura ya 442 imebainisha sekta ambazo malipo yanayofanyika katika sekta hizo yanapaswa kufanyika kwa njia za kidijitali kuanzia Julai 2026.
Licha ya Sheria ya Miamala ya Kielektroniki, Serikali pia, imetoa miongozo kwa sekta mbalimbali ili kutumia mifumo ya kidigitali katika shughuli mbalimbali za sekta husika.
Kwa upande wa sekta ya mawasiliano, maeneo ambayo tunatakiwa kuanza nayo kwa mujibu wa miongozo hiyo ya serikali ni katika kuongeza muda wa maongezi ya simu ambapo vocha za muda wa maongezi zinapaswa kununuliwa kwa njia za kidigitali. Lengo kuu ni kuhamasisha uchumi usiotumia fedha taslimu na unaotumia mifumo ya kidijitali lakini kwa upande mwingine kupunguza taka zitokanazo na kadi za kukwangua za muda wa maongezi ya simu ili kulinda mazingira na afya za binadamu na wanyama.

Ni faida gani wananchi wanatarajiwa kupata kutokana na mabadiliko haya?
Kupunguza/kuondoa malipo kwa kutumia fedha taslimu.
Kutunza mazingira kwa kupunguza uzalishaji, usambazaji na utupaji wa kadi halisi za kukwangua za muda wa maongezi pamoja na athari zake kwa mazingira, huku ukiunga mkono maendeleo ya sekta ya mawasiliano yenye ufanisi zaidi na inayotumia teknolojia za kidijitali.
Kuongeza ufanisi ambapo wateja wanaweza kuongeza salio kwa urahisi, ndani ya muda mfupi, wakati wowote ule na mahali popote maadam tu kuna upatikanaji wa mifumo husika ya kununua muda wa maongezi kidijitali. Hivyo mteja anaweza kuendelea na shughuli zake zozote za kiuchumi, bila kwenda umbali fulani kwa ajili tu ya kutafuta vocha ya kukwangua ya muda wa maongezi na hivyo kuongeza ufanisi katika shughuli zao.
Kuimarisha usalama na ulinzi wa watumiaji kwa kupunguza hatari ya kuibiwa kwa vocha, kuharibika kwa namba za siri za vocha, kufichuliwa kwa namba za kuongeza salio za vocha na kusambazwa kwa vocha bandia.
Baada ya kuondolewa kwa kadi za kukwangua, wananchi wataongezaje muda wa maongezi?
Watoa huduma wa mawasiliano ya simu wameweka utaratibu wa kuongeza muda wa maongezi kwa njia ya kidijitali ambapo wa sasa wananchi wanaweza kutumia njia zifuatazo: -
Kununua muda wa maongezi moja kwa moja kupitia akaunti zao za miamala ya fedha za simu kwa kutumia huduma za USSD au programu za simu (application);
Mawakala wa huduma za fedha za simu;
Mashine za kujihudumia za benki (ATM) na mawakala wa benki; na
Mifumo mingine ya kidijitali ya kuongeza muda wa maongezi inayotolewa na Watoa Huduma wa Mitandao ya Simu na washirika wao walioidhinishwa.
Wananchi wanaweza kupata taarifa Zaidi kwa kuwasiliana na mtoa huduma wako kupitia namba 100 ambayo ndio namba pekee inayotumika kuwasiliana kati ya mtoa huduma na mteja pale watakapopata changamoto yoyote.

Je, kutakuwa na njia mbadala kwa wananchi ambao hawana simu janja?
Watumiaji wa huduma za mawasiliano ya simu ambao hawana simu janja wanaweza kutumia njia zifuatazo:-
Kununua muda wa maongezi moja kwa moja kupitia akaunti za fedha za simu kwa kutumia huduma za USSD na
Kutumiamawakala wa watoa huduma wa fedha za simu na mabenki;
Mashine za kujihudumia za benki (ATM).
Je, kuhamia kwenye mfumo wa kidijitali kutabadilisha bei za vifurushi au muda wa maongezi?
Hapana kununua muda wa maongezi kwa njia za kidijitali hakutabadirisha bei za vifurushi au bei muda wa maongezi. Mpaka sasa wanannchi wote wanaonunua muda wa maongezi kwa njia ya kidijitali hufanyika bure bila gharama au makato yoyote.
Je, wananchi wa maeneo yasiyo na huduma nzuri ya intaneti watawezaje kuongeza muda wa maongezi?
Tunaposema kuongeza muda wa maongezi kidijitali hatumaanishi lazima kuwe na huduma ya intaneti. Kwa hiyo kwa maeneo ambayo hamna huduma ya intaneti maadamu kuna huduma za simu kama 2G au kwa watumiaji wanaotumia viswaswadu (simu ambazo sio simu janja) wanaweza kununua kwa kutumia USSD kama mtu anataka kujihudumia yeye mwenyewe toka kwenye simu yake au kuwaona mawakala wa wa watoa huduma wanaotoa huduma za fedha za simu ili kuongeza muda wa maongezi endapo hataki kujihudumia mwenyewe.
Kwa wale wenye simu janja ambao wangependa kutumia application za kuongeza muda wa maongezi, hao ndiyo wanahitaji kuwa na huduma za intaneti ili kuongeza muda wa maongezi kidijitali, ambapo nao pia kama kunakuwa na changamoto ya inteneti anaweza tumia USSD au kutumia mawakala.
Je Kadi za kukwangua za muda wa maongezi zilizo mikononi mwa watumiaji wa Huduma za Mawasilano zitaendelea kutumika?
Watumiaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo ya majaribio ambao watakuwa bado wana kadi za kukwangua za muda wa maongezi ya simu ambazo zitakuwa hazijatumika baada ya tarehe 1 Januari 2027, watahitajika kuwasiliana na Watoa Huduma wao kupitia vituo vya huduma kwa wateja au vituo vya huduma vilivyoidhinishwa kwa ajili ya kupata msaada na kuwezesha kadi hizo kutumika. Utaratibu huu ni kama ule ulipo sasa endapo kwa bahati mbaya mtu amekwangua vibaya vocha yake na baadhi ya namba kutoonekana, basi akimpigia mtoa huduma na kumtajia serial namba ya kadi husika basi mtoa huduma huongeza muda husika moja kwa moja kwa mtumoiaji husika.
Hata hivyo, tunawahimiza watumiaji wa huduma za mawasiliano ya simu katika maeneo ya majaribio wanashauriwa kutumia kadi zao za kukwangua za muda wa maongezi ya simu walizonazo kabla ya tarehe 1 Januari 2027 na kuanza kutumia njia za kidijitali za kuongeza muda wa maongezi ya simu. Akishaongeza muda wake kabla ya muda huo, muda huo utaendelea kukaa kwenye simu yake mpaka pale atakapoamua kuutumia. Kitu cha msingi kwa watumiaji wanaotumia vifurushi vya muda wa maongezi ni kuhakikisha wamesitisha matumizi ya muda wa maongezi wa kawaida baada ya vifurushi vyao kuisha ili kuondoa uwezekano wa salio lao kutumika baada ya vifurushi husika kuisha.

Je, wafanyabiashara wanaouza kadi za kukwangua wataathirika vipi na mabadiliko haya?
Wafanya biashara wanaouza kadi za kukwangua za muda wa maongezi ya simu hawataathirika na zoezi hili bali wataendelea kutoa huduma hii kwa njia za kidijitali. Katika maeneo mengi ya mijini, wafanyabiashara wengi hawana kadi za vocha za kukwangua na endapo mtumiaji atafika katika maeneo yao na kuulizia vocha ya kukwangua ataambiwa huduma iliyopo ni ya kidijitali isipokuwa kwa sehemu chache ambazo bado wanatoa huduma za vocha za kukwangua, ambao nao baada ya zoezi hili watahamia kwenye kuongeza muda wa maongezi kwa njia za kidijitali.
Pia tusisahau kuwa watoa huduma hawataendelea kutoa vocha za kukwangua kwa mawakala wao na wataendelea kuwawezesha mawakala hao kutoa huduma kusika kwa njia za kidijitali kama mbadala wa njia ya awali ya vocha za kukwangua.
Aidha, Wananchi walio nje ya maeneo ya majaribio kwa Kanda ya Kaskazini tunawahimiza pia kuanza kutumia njia za kidijitali kujiandaa na utekelezaji wa mpango huu kitaifa. TCRA kwa kushirikiana na kampuni za simu itaendelea kutoa elimu na mwongozo ili kuhakikisha wananchi wanaelewa mabadiliko haya na namna ya kutumia njia mbadala.
0 Comments