Na OWM-TAMISEMI, Mwanza
NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Dkt.Festo Dugange, amesema Serikali imetumia Shilingi Bilioni 604.6 kujenga shule mpya za msingi 676 na matundu ya vyoo 34,464 katika kipindi cha miaka minne, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji nchini.
Dkt.Dugange ameyasema hayo Novemba 10, 2026, alipotembelea na kukagua utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji wa Elimu ya Awali na Msingi (BOOST) katika Shule ya Msingi Isamilo, wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza.
Amesema uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha watoto wanapata elimu bora kwa kusoma katika mazingira rafiki na yenye miundombinu inayokidhi mahitaji yao.
Akizungumzia mafanikio ya mradi huo katika shule hiyo, Dkt. Dugange amesema Serikali ilitoa takribani Shilingi Milioni 541 zilizotumika kujenga madarasa zaidi ya 14, yanayotumiwa na wanafunzi 1,336.
Amesema ujenzi huo umechangia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuonesha dhamira ya Serikali katika kuimarisha sekta ya elimu nchini.
"Watoto wetu 1,336 wanasoma katika shule nzuri na bora ya Msingi Isamilo. Kama ambavyo Serikali imekuwa ikieleza siku zote, inawajali watoto wetu kwa kujenga shule bora na kuhakikisha wanasoma katika mazingira mazuri," amesema.
Aidha, Dkt.Dugange amesema kupitia mradi wa BOOST, Serikali imewekeza zaidi ya Shilingi Trilioni 1.15, ambapo madarasa zaidi ya 16,000 yamejengwa ili kuongeza upatikanaji wa elimu bora na kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za elimu ya awali na msingi.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya elimu ili kuwawezesha wanafunzi kupata mazingira bora ya kujifunzia na walimu kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.



0 Comments