TANROADS Mkoa wa Shinyanga yapokea agizo hilo kwa utekelezaji; usanifu wa kina wa barabara yenye urefu wa kilomita 54 unatakiwa kukamilika kabla ya maandalizi ya bajeti mpya.
Na Neema Nkumbi, Kahama
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameiagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuharakisha na kukamilisha usanifu wa kina wa barabara ya Kahama–Ushetu yenye urefu wa takribani kilomita 54, ili iweze kuzingatiwa katika maandalizi ya bajeti mpya ya miradi ya barabara.
Agizo hilo limepokelewa kwa ajili ya utekelezaji na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga, kufuatia kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Ushetu wanaohitaji barabara hiyo kujengwa kwa kiwango cha lami ili kurahisisha usafiri na kuchochea shughuli za kiuchumi.
Waziri Mkuu ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara yake Halmashauri ya Ushetu, mkoani Shinyanga, baada ya Mbunge wa Jimbo hilo, Emanuel Cherehani, kuwasilisha ombi la ujenzi wa barabara hiyo, akieleza kuwa eneo hilo bado linahitaji mradi mkubwa wa kimkakati wa barabara.
Akifuatilia hatua za maandalizi ya mradi huo, Dkt. Mwigulu ameuliza kuhusu maendeleo ya usanifu na kuelezwa kuwa mapitio ya usanifu wa awali yanaendelea, huku usanifu wa kina ukitarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu.
Hata hivyo, ametaka muda huo upunguzwe na kazi ikamilike kabla ya maandalizi ya bajeti mpya, akisisitiza umuhimu wa TANROADS kufanya kazi kwa kasi ili barabara hiyo isiendelee kukwama katika hatua za maandalizi.
“Nimewaelekeza mpunguze muda huo na kuhakikisha usanifu wa kina unakamilika kabla ya maandalizi ya bajeti mpya, Fanyeni kazi usiku na mchana ili barabara hii iweze kuzingatiwa pamoja na miradi mingine mipya ya barabara,” anesema Dkt. Mwigulu.
Ameonya kuwa Serikali haitaki kufika wakati wa maandalizi ya miradi mipya na kukutana na kisingizio kwamba usanifu wa barabara hiyo haujakamilika.
Waziri Mkuu ameeleza kuwa Serikali inaendelea na utaratibu wa kurejesha wakandarasi kwenye miradi iliyokwama kutokana na changamoto za fedha, kulipa malipo ya awali kwa wakandarasi wenye mikataba iliyosainiwa kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi mipya.
Awali, Cherehani amesema barabara hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya Ushetu na kwamba wananchi wako tayari ujenzi wake ufanyike kwa awamu endapo Serikali haitakuwa na uwezo wa kujenga kilomita zote 54 kwa wakati mmoja.
Ameeleza kuwa maeneo mengine ya Msalala na Manispaa ya Kahama yamepata barabara za kimkakati kwa kiwango cha lami, hivyo Ushetu nayo inahitaji kupewa kipaumbele katika mipango ya Serikali.
Kwa sasa, hatua muhimu inayosubiriwa ni TANROADS kukamilisha usanifu wa kina kwa muda uliopangwa, ili kuweka msingi wa kuingizwa kwa mradi huo katika mipango na bajeti za Serikali.

0 Comments