Aahidi kukutana na wabunge wa maeneo yanayoathirika kujadili gharama za pembejeo; wakulima wa Ushetu walalamikia riba na makato yanayoongeza gharama za uzalishaji.
Na Neema Nkumbi, Kahama
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameelekeza kufanyika kwa mapitio ya tozo na gharama zinazohusiana na upatikanaji wa pembejeo za kilimo, kufuatia malalamiko ya wakulima wa tumbaku kuhusu gharama kubwa za uzalishaji zinazopunguza manufaa wanayopata kutokana na kilimo hicho.
Amesema Serikali itakutana na wabunge kutoka maeneo yanayoathirika na changamoto hizo ili kujadili na kutafuta ufumbuzi, akisisitiza kuwa Serikali inalenga kutoa majibu ya kero zinazowakabili wananchi badala ya kuziacha ziendelee.
Dkt. Mwigulu ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake katika Halmashauri ya Ushetu, mkoani Shinyanga, baada ya kupokea hoja za Mbunge wa Jimbo hilo, Emanuel Cherehani, aliyeeleza changamoto zinazowakabili wakulima wa tumbaku, ikiwamo gharama za pembejeo na mfumo wa riba unaodaiwa kuwabebesha mzigo zaidi.
“Nataka tukutane na wabunge wanaotoka katika maeneo haya yanayoathirika na mambo haya ya pembejeo, ili tuweze kuhakikisha kwamba hoja ya Cherehani ambayo ameileta tunapata ufumbuzi, Hii ni Serikali inayotoa majibu,” amesema Waziri Mkuu.
Katika maelezo yake, Cherehani amesema kilimo cha tumbaku ni tegemeo la wananchi wengi wa Ushetu, akieleza kuwa takribani asilimia 99 ya wakazi wa eneo hilo wanategemea shughuli zinazohusiana na zao hilo.
Amesema pamoja na mchango wa tumbaku katika uchumi wa kaya na wilaya, wakulima wanakabiliwa na changamoto ya bei wanazolipwa pamoja na gharama za pembejeo zinazohitajika katika uzalishaji.
Miongoni mwa hoja alizowasilisha ni mfumo wa riba unaodaiwa kusababisha mkulima na msambazaji wa pembejeo kubebeshwa gharama za riba zinazohusiana na mfuko mmoja wa mbolea, hali inayoongeza gharama kwa wakulima.
Waziri Mkuu amesema amepokea hoja hiyo na kuelekeza mawaziri wenye dhamana ya fedha, kilimo na utawala wa Serikali za Mitaa kushirikiana katika kupitia changamoto hizo ili kubaini namna bora ya kuzitatua.
Hatua hiyo inakuja wakati wakulima wanahitaji mazingira yanayowawezesha kupata pembejeo kwa gharama nafuu na kuuza mazao yao kwa bei inayozingatia gharama za uzalishaji.
Katika hoja nyingine inayohusu sekta ya kilimo, Waziri Mkuu alizungumzia hatua zilizochukuliwa kuhusu ununuzi wa pamba, akieleza kuwa vikwazo vilivyokuwa vinazuia uwepo wa wanunuzi wengi vimeondolewa katika msimu husika ili kuongeza ushindani na kuwapa wakulima nafasi ya kupata bei nzuri.
Aidha, ameeleza kuwa Serikali imepokea malalamiko kuhusu utaratibu wa utaifishaji wa mifugo, na kwamba sheria iliyokuwa ikiruhusu hatua hiyo imefutwa kufuatia maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa wakulima wa Ushetu, utekelezaji wa mapitio yaliyoagizwa na Waziri Mkuu utakuwa muhimu katika kubaini iwapo gharama za pembejeo zitapungua na kama mfumo wa upatikanaji wake utawekwa katika mazingira yanayowanufaisha zaidi wazalishaji.




0 Comments