Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

USHETU YAPOKEA SH1.04 BILIONI, NYUMBA TATU ZA WAKUU WA IDARA KUJENGWA





NA NEEMA NKUMBI, USHETU




Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu mkoani Shinyanga imepokea Sh bilioni 1.04 kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi sita ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa nyumba tatu za wakuu wa Idara, ukamilishaji wa vituo vya afya na ununuzi wa vifaa tiba.

Akizungumza na DADAVUA MEDIA pamoja na Huheso Digital, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Bi. Hadija Kabojela, amesema fedha zote tayari zimepokelewa na kwamba kila mradi unapokea fedha moja kwa moja katika kituo au eneo husika la utekelezaji.

Amesema katika fedha hizo, Sh milioni 450 zimeelekezwa katika ujenzi wa nyumba tatu za wakuu wa Idara, zitakazojengwa katika Kata ya Nyamilangano, ambapo kila nyumba itagharimu Sh milioni 150.

Kwa mujibu wa Kabojela, kwa sasa Halmashauri inaendelea na hatua za kumpata mkandarasi atakayetekeleza mradi huo, ambaye baada ya kupatikana atafuata taratibu za kimkataba kabla ya kuanza kwa ujenzi.

Katika sekta ya afya, Sh milioni 100 zimeelekezwa katika ukamilishaji wa Kituo cha Afya Nyalwelwe na Sh milioni 100 nyingine kwa ajili ya ukamilishaji wa Kituo cha Afya Igwamanoni.

Akifafanua kuhusu fedha hizo, Kabojela amesema siyo kwa ajili ya ukarabati wa majengo yaliyopo, bali ni kukamilisha majengo yaliyosalia ili vituo hivyo viweze kukamilika.

Aidha, amesema Sh milioni 50 zimeelekezwa katika ununuzi wa vifaa tiba kwa Zahanati ya Bugela, ambapo vifaa vinavyotarajiwa kununuliwa ni pamoja na vifaa vya uzalishaji kwa wajawazito, vifaa vya maabara kama hadubini, pamoja na vifaa vya uchunguzi wa awali ikiwemo vipimajoto na mizani za kupimia uzito.

Amesema kabla ya ununuzi huo, kutafanyika tathmini ili kubaini vifaa ambavyo havipo au vinavyohitajika kwa umuhimu zaidi, hatua itakayosaidia kuhakikisha fedha hizo zinatumika kununua vifaa vinavyokidhi mahitaji ya zahanati hiyo.

Katika kuboresha mazingira ya utendaji wa Halmashauri, Sh milioni 300 zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa samani za jengo la Utawala, huku Sh milioni 40 zikielekezwa katika usimamizi na ufuatiliaji wa miradi yote inayotekelezwa na halmashauri hiyo12.

Kuhusu muda wa utekelezaji, Kabojela amesema maelekezo ya Serikali ni kuhakikisha miradi hiyo, ikiwemo ujenzi wa nyumba na ukamilishaji wa vituo vya afya, inatekelezwa ndani ya mwaka wa fedha 2026/2027.

Amesisitiza kuwa fedha hizo zimepokelewa katika maeneo husika ya utekelezaji, hivyo hatua zinazofuata ni kuhakikisha taratibu zinakamilika na miradi inaanza kutekelezwa kwa kuzingatia malengo yaliyokusudiwa.


Fedha zimetolewa, sasa macho ya wananchi yaelekezwe kwenye matokeo.

Endelea kufatilia www.dadavuamedia.co.tz na Huheso.co.tz kwa taarifa zaidi


Post a Comment

0 Comments