Na Neema Nkumbi, Kahama
Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Mhe. Shabani Mikongoti, ameteuliwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Chama cha Skauti Tanzania Wilaya ya Kahama, hatua inayompa nafasi ya kushiriki katika uongozi na kusimamia maendeleo ya chama hicho katika wilaya.
Kwa mujibu wa barua ya uteuzi iliyotolewa Novemba 5, 2026 na Kamishna wa Skauti Mkoa wa Shinyanga, Mussa M. Chama, uteuzi huo ulifanyika kufuatia kikao cha Kamati Tendaji pamoja na Bodi ya Mkoa kilichoketi Oktoba 9, 2026.
Barua hiyo imeeleza kuwa uteuzi wa Mhe. Mikongoti ulianza rasmi Oktoba 10, 2026 kwa mujibu wa Katiba ya Chama cha Skauti Tanzania.
Hata hivyo, utekelezaji rasmi wa majukumu yake utaanza baada ya kula kiapo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Dkt. Francis Daudi, ambaye pia ni Mlezi wa Skauti wa Wilaya hiyo.
Akitoa ujumbe wa shukrani kufuatia uteuzi huo, Mhe. Mikongoti ameupongeza uongozi wa Chama cha Skauti Tanzania Mkoa wa Shinyanga kwa kumwamini na kumpa nafasi hiyo, akiahidi kushirikiana na viongozi wengine katika kuendeleza malezi ya vijana, kukuza maadili na kuimarisha chama.
Uteuzi huo unakuja wakati ambapo malezi ya vijana, uzalendo, nidhamu na uwajibikaji ni maeneo muhimu yanayohitaji ushiriki wa viongozi na wadau mbalimbali katika jamii.
DADAVUA MEDIA inaendelea kufuatilia masuala ya uongozi na maendeleo ya jamii katika Manispaa ya Kahama.
Endelea kutufuatilia kupitia www.dadavuamedia.co.tz

0 Comments