Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HOSPITALI YA MANISPAA YA KAHAMA YAHUDUMIA WAGONJWA ZAIDI YA 211,000 KWA MWAKA, YATAJA CHANGAMOTO





Na Neema Nkumbi, Kahama

Hospitali ya Manispaa ya Kahama imehudumia jumla ya wagonjwa 211,314 mwaka 2025, huku ikiendelea kukabiliwa na changamoto za upungufu wa watumishi, miundombinu na vifaa tiba kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma za afya kutoka kwa wananchi wa Manispaa ya Kahama na maeneo jirani.

Takwimu hizo zimetolewa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dkt. Michael John Mushi, wakati akiwasilisha taarifa ya utendaji wa hospitali katika hafla ya watumishi iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Naibu Meya wa Manispaa ya Kahama aliyemwakilisha mgeni rasmi, Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini, Benjamin Ngayiwa.

Akiwasilisha taarifa hiyo, Dkt. Mushi amesema hospitali hiyo iliyoanzishwa mwaka 1974 imeendelea kupiga hatua katika kuboresha huduma za afya, ikiwemo kukamilika kwa ujenzi wa kliniki ya Methadone kwa ajili ya huduma kwa watu wenye changamoto ya matumizi ya dawa za kulevya, pamoja na jengo na mitambo ya kuzalisha hewa tiba ya oksijeni ambayo tayari imeanza kutoa huduma.

Amesema hospitali hiyo pia imepokea vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 269 kupitia Serikali Kuu na mradi wa TIMCHIP, pamoja na Sh milioni 100 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba, huku ikiendelea kutumia mapato ya ndani kuboresha miundombinu na huduma za Mama na Mtoto, Bima ya Afya na Fast Track.

Katika hatua nyingine, amesema hospitali imepokea Sh milioni 660 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa mahututi wachanga (NICU) na jengo la kichomea taka za hospitali, hatua inayotarajiwa kuongeza uwezo wa hospitali katika kutoa huduma bora na salama.

Hata hivyo, amesema hospitali inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa watumishi, ambapo kwa sasa ina watumishi 465 ambao hawakidhi mahitaji ya utoaji huduma kulingana na idadi ya wagonjwa wanaohudumiwa.

Amesema hali hiyo imeifanya hospitali kutumia mapato ya uchangiaji kuajiri baadhi ya watumishi wa mikataba na kutumia watumishi wa kujitolea ili kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa.

Ameongeza kuwa mahitaji mengine muhimu ni ujenzi wa jengo la dharura na wagonjwa mahututi (Emergency Department na ICU), upatikanaji wa mashine ya CT-Scan, ujenzi wa wodi mpya pamoja na jengo la huduma za Bima ya Afya, huku ujenzi wa jengo la ghorofa tatu ukiendelea kwa lengo la kuongeza nafasi za kutolea huduma.

Dkt. Mushi amesema lengo la hospitali hiyo ni kuendelea kuimarisha huduma na miundombinu ili kufikia vigezo vya kupandishwa hadhi na kuwa Hospitali ya Rufaa, akitoa wito kwa viongozi na wadau kushirikiana katika kutatua changamoto zilizopo.

Kwa upande wake, Naibu Meya wa Manispaa ya Kahama, akizungumza kwa niaba ya mgeni rasmi, Mbunge Benjamin Ngayiwa, amewataka watumishi wa hospitali hiyo kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kujituma na kuzingatia maadili ya taaluma zao ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya.

Amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya afya kwa kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu na huduma, hivyo watumishi wanapaswa kuunga mkono juhudi hizo kwa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kujituma.

Ameeleza kuwa pamoja na uwekezaji huo, bado zipo changamoto za upungufu wa watumishi, fedha na rasilimali nyingine muhimu, zinazohitaji ushirikiano wa viongozi, watendaji na wadau mbalimbali ili kupata ufumbuzi.

Aidha, amewapongeza watumishi wa hospitali hiyo kwa kujitoa katika kuwahudumia wananchi licha ya mazingira yenye changamoto, akisisitiza kuwa kazi wanayoifanya ina mchango mkubwa katika kulinda na kuimarisha afya za jamii.

Hospitali ya Manispaa ya Kahama inatoa huduma kwa wakazi wa Manispaa ya Kahama pamoja na wananchi kutoka Halmashauri za Msalala na Ushetu na maeneo jirani, ikiwemo baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Geita.

Post a Comment

0 Comments