Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Frank Nkinda (kushoto), akimkabidhi ofisi rasmi Mkuu mpya wa Wilaya ya Kahama, Dk. Francis Mlacha (kulia)

NA NEEMA NKUMBI, KAHAMA
Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, amemkabidhi rasmi Mkuu mpya wa Wilaya hiyo, Dk. Francis Mlacha, ofisi hiyo huku akimtaka kuweka nguvu katika kulinda haki za wananchi wanyonge na kukabiliana na changamoto zinazowakabili.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo, Oktoba 5, 2026, baada ya Nkinda kuhamishwa na kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, huku Dk. Mlacha akiteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kahama.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Nkinda amesema changamoto kubwa aliyokutana nayo kwa mwananchi wa Kahama ni suala la haki, akidai kuwa baadhi ya watu wenye uwezo wa kifedha wamekuwa wakitumia nguvu ya fedha katika masuala yanayohusu haki za wananchi wanyonge.
“Asilimia kubwa ya watu wenye fedha Kahama wanaamini fedha kuliko haki za wanyonge, Kilio kikubwa cha wanyonge Kahama ni kukosa haki na hawana furaha, Nakuombea sana katika hili, niwaombe na wazazi wako, mumuombee sana kijana mwenzangu, kwa maombi yenu ataweza,” amesema Nkinda.
Nkinda amemtaka Dk. Mlacha kutumia nafasi yake kusimamia haki, akirejea mafundisho ya Biblia yanayosisitiza viongozi kufungua vinywa vyao kwa ajili ya wasio na uwezo wa kujitetea.
Ametaja Mithali 31:8-9 inayowataka viongozi kuwatetea wasiojiweza na kuwapatia haki maskini na wahitaji, huku pia akirejea Isaya 1:17 unaosisitiza kutenda mema, kutafuta haki na kuwasaidia wanaoonewa.
Aidha, ametumia Zaburi 82:3-4 kusisitiza wajibu wa kutenda haki kwa maskini na yatima, kuwaokoa wahitaji na kuwalinda dhidi ya wanaowadhulumu.
Mbali na suala la haki, Nkinda amemtaka mkuu huyo mpya kuwa tayari kukabiliana na changamoto ya wizi wa mita za maji ambao, kwa mujibu wake, ulikuwa umedumu kwa zaidi ya mwaka mmoja kabla ya kuchukuliwa hatua.
Amesema katika harakati za kukomesha wizi huo, mamlaka zilifanikiwa kuwakamata baadhi ya wahusika, lakini uchunguzi ulionyesha kuwa kulikuwa na watu wenye ushawishi waliokuwa nyuma ya uhalifu huo.
“Nilipokuja Kahama changamoto ya wizi wa mita za maji ilikuwa na miezi kumi nyuma bila ufumbuzi, Tulipambana tukawakamata wahalifu, lakini tukagundua nyuma kuna vigogo, Ilikuwa shughuli kweli na vita ilikuwa ni kubwa, simu nyingi, maelekezo mengi, Nikasema liwalo na liwe, tulisimama kweli kwa maslahi ya wananchi ili kuimarisha mahusiano mazuri kati ya wananchi na Serikali yao,” amesema.
Changamoto nyingine aliyomkabidhi Dk. Mlacha ni migogoro ya ardhi, ambayo amesema imekuwa ikihusisha baadhi ya watu wenye uwezo wa kiuchumi wanaodhani wanaweza kutumia uwezo wao kufanya lolote.
“Jambo la pili ni migogoro ya ardhi, Kahama ni moja ya maeneo ambayo baadhi ya watu wenye uwezo kiuchumi wanaamini wanaweza kufanya chochote, Kwa kushirikiana na kamati yangu tumepambana, Jiandae kisaikolojia, haya utakutana nayo, na yanasababishwa na baadhi ya watumishi wetu wa Manispaa,” ameongeza Nkinda.
Kwa upande wake, Mkuu mpya wa Wilaya ya Kahama, Dk. Francis Mlacha, amesema atahakikisha anaendeleza mazuri yaliyoanzishwa na mtangulizi wake, akisisitiza usimamizi madhubuti wa miradi ya maendeleo.
Dk. Mlacha amesema moja ya maeneo atakayoyapa kipaumbele ni kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinatumika kwa thamani inayolingana na kiasi kilichotolewa.
“Kwa kushirikiana na kamati yangu tutahakikisha tunasimamia miradi ya maendeleo inayoanzishwa iendane na thamani ya fedha zinayotolewa, kwa sababu tukiacha darasa lisijengwe kwa viwango, atakayeangukiwa na matofali ni mtoto wetu, Mimi niko tayari kufanya kazi na nyinyi,” amesema Dk. Mlacha.











0 Comments