Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NGAYIWA ATOA WITO WA KUUNGA MKONO UJENZI NA UPANUZI WA MISIKITI KAHAMA MJINI





Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini, Benjamin Ngayiwa, ametoa wito kwa wadau na wananchi kushirikiana katika kuunga mkono juhudi za upanuzi na ujenzi wa misikiti ili kuboresha mazingira ya ibada kwa waumini wa dini ya Kiislamu.

Ngayiwa ametoa wito huo baada ya kutembelea na kupokea taarifa za mahitaji ya Misikiti ya Ikh-Laswi, iliyopo Mbulu, na Rufida, iliyopo Majengo, katika Manispaa ya Kahama.

Katika Msikiti wa Ikh-Laswi, Imam wa msikiti huo, Sadam Haruna Yusuph, ameeleza kuwa msikiti unahitaji kuongeza eneo lake kwa kununua viwanja vinavyouzunguka ili kupanua nafasi ya waumini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa, gharama za ununuzi wa maeneo hayo zinakadiriwa kufikia shilingi milioni 50, huku kiasi cha shilingi milioni 14.5 kikiwa tayari kimepatikana kwa ajili ya kutekeleza lengo hilo.

Kwa upande wa Msikiti wa Rufida, uliopo Majengo, Imam Mkuu wa msikiti huo, Sheikh Mwamfundo Juma, ameeleza mpango wa kujenga msikiti mpya wa kisasa wenye ghorofa moja, utakaoboresha mazingira ya ibada kwa waumini.

Ujenzi wa msikiti huo unakadiriwa kugharimu shilingi milioni 360, kiasi kinachohitaji ushirikiano wa waumini na wadau mbalimbali katika kufanikisha mradi huo.

Akizungumza katika ziara hiyo, Ngayiwa amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi wa dini, waumini na wadau wa maendeleo katika kutekeleza miradi inayolenga kuboresha huduma za kijamii na mazingira ya ibada.

Hatua hiyo inalenga kuimarisha juhudi za upanuzi wa maeneo ya ibada na ujenzi wa miundombinu ya kisasa inayokidhi mahitaji ya waumini katika Jimbo la Kahama Mjini.

Post a Comment

0 Comments