Katibu wa chama cha mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kahama Andrew Chatwanga akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi yake Kahama.
Na Neema Nkumbi Kahama, Shinyanga
Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kahama kimewatoa onyo kali kwa
wanachama wanaotia nia ya kugombea nafasi za udiwani na ubunge, wanaoanza
kampeni za chinichini kwa kutoa hongo kwa wajumbe kabla ya mchakato rasmi wa
uchaguzi kuanza.
Akizungumza na waandishi wa habari may 8, 2025 Katibu wa CCM Wilaya ya
Kahama, Ndg. Andrew Chatwanga, amesema kuwa chama kimepokea taarifa za
kuwepo kwa baadhi ya watia nia wanaowaita wajumbe wa mkutano mkuu na
kuwapa fedha kiasi cha shilingi elfu kumi kwa kila mmoja, kitendo
ambacho ni kinyume na maadili, kanuni na taratibu za chama hicho.
"Chama cha Mapinduzi kimeweka utaratibu mzuri sana wa kugombea, lakini
baadhi ya watia nia wameanza kutoa hongo kwa wajumbe, hiyo siyo CCM
tunayoitaka. Kuwapa watu elfu kumi ni kuwadhalilisha wanachama wetu na
kudhoofisha taswira ya chama," amesema Chatwanga.
Chatwanga amefafanua kuwa mchakato rasmi wa kugombea utaanza kwa kuchukua
fomu, kisha kufuatiwa na vikao halali vya chama ambavyo vitapitia majina ya
wagombea na hatimaye kuwasilisha majina matatu kwa Kamati Kuu ya Taifa kwa
ajili ya uteuzi.
“Watu wanaweza kuchukua fomu hata mia moja, lakini mwisho wa siku ni majina
matatu pekee yatakayochaguliwa na kupelekwa kwa ajili ya kura za maoni,
Rushwa si kigezo cha kupata nafasi katika CCM. Kiongozi bora ni yule
anayeishi na wananchi, anayejua matatizo yao na anayetambulika kwa
uadilifu," ameongeza Chatwanga.
Aidha, amewataka wale wote wanaofanya mikutano ya siri usiku na kutoa fedha
kwa wajumbe kuacha mara moja, akisema chama kina taarifa na majina yao yote
hivyo hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kukiuka taratibu
hizo.
"Chama kitachukua hatua kali kwa wale wote wanaokiuka maadili, Ubunge na
udiwani ni nafasi za uwakilishi, si biashara ya fedha, Tunataka wagombea
wanaotokana na mapenzi ya wananchi, si wale wanaonunua nafasi kwa njia ya
rushwa," amesema Chatwanga.
Katibu huyo amesisitiza kuwa wabunge waliopo madarakani waachwe wafanya
kazi zao hadi muda wao utakapomalizika, na kwamba vitendo vya hujuma na
mikakati ya kuwahujumu havitavumiliwa.



0 Comments